Taarifa ya Serikali - Kuzama kwa Meli Zanzibar
MAAFA YA KUZAMA KWA MELI ZANZIBAR
Meli ya Mv. Star Gate imezama karibu na Kisiwa cha Chumbe ambapo watu 12 wamefariki
hadi muda huu na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Akitoa taarifa fupi kwa waandishi wa habari,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini alisema taarifa
za kuzama kwa meli hiyo ilitolewa na Boti iendayo kasi ya Kilimanjaro III
iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar ndipo ilipoiona meli hiyo
ikizama.
“Tulipata taarifa kutoka Boti ya abiria ya Kilimanjaro III saa 7:50 mchana
waliporipoti kuona meli ikizama karibu na Kisiwa cha Chumbe” Alisema Waziri
Mwinyihaji.
Waziri huyo alisema Meli hiyo imezama maili sita kuelekea Kisiwa cha Yasin
Kusini mwa Kisiwa cha Chumbe kilichopo Unguja maili kadhaa kutoka Bandari ya
Malindi.
Waziri Mwinyihaji alisema idadi ya abiria walikuwa 250 ambao ni watu wazima,
watoto 31 na mabaharia 6. “Tumepeleka waokoaji, kuna boti tano zipo eneo la
tukio kushirikiana na waokoaji wengine” Alisema Waziri Mwinyihaji.
Alisema maiti zote zitapelekwa viwanja vya Maisara Zanzibar kwa ajili ya
ndugu na jamaa kuzitambua maiti za ndugu zao ambapo majeruhiwa wote watatibiwa
Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Katika Bandari ya Malindi mwandishi wetu ameshuhudia maiti kadhaa zikiwemo
za watoto zikishushwa, Miongoni mwa abiria waliookolewa ni raia 13 wa Mataifa
mbalimbali ya nje huku raia mmoja ambaye hakuweza kutambuliwa utaifa wake amepoteza maisha.
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alifika eneo la
Bandari ya Malindi Zanzibar pamoja viongozi wengine akiwemo Spika wa Baraza la
Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Mawaziri na
baadhi ya Wajumbe a Baraza la Wawakilishi walikuwepo kutoa msaada unaohitajika.
Katika eneo la pembezoni mwa bandari ya Malindi, makundi ya wananchi
yalikuwa yamekusanyika wakisubiri taarifa za tukio hilo tangu saa 8:30 mchana.
Vikosi vya ulinzi na usalama, msalaba mwekundu na watoaji wengine wa
misaada ya dharura walifika kwa haraka eneo la tukio.
Hadi sasa kazi ya
uokoaji inaendelea karibu na Kisiwa cha Yasin ilikozama meli hiyo.
Meli ya Mv. Star
Gate inamilikiwa na kampuni ya kizalendo ya Sea Gull Sea Transport Ltd ambayo
mwaka 2009 Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilipinduka na kuzama katika Bandari
ya Malindi Zanzibar na kua watu sita.
Mwaka jana Zanzibar ilikumbwa na maafa baada ya Meli ya Mv. Spice Islanders
kuzama katika bahari ya Hindi eneo la Nungwi katika Kisiwa cha Unguja ikielekea
Kisiwani Pemba ambapo taarifa rasmi ya Serikali ilisema watu 197 walipoteza
maisha na wengine wengi kujeruhiwa.
Taarifa zaidi zitatolewa hapo baadea.
Imetolewa na:
Idara ya Habari(MAELEZO) Zanzíbar
Julia 18,2012
Zanzíbar,Tanzania
No comments:
Post a Comment