Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania,
Dk. Valentino Mokiwa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, imetoa amri ya kukamatwa kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, kwa maelezo kuwa amekaidi amri ya mahakama iliyokataza kusimikwa kwa Askofu mteule wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Stanley Kanso Hotai.
Pia, mahakama imeagiza kukamatwa kwa Hotai, ambaye ni mdaiwa wa pili kwa kuidharau mahakama.
Hatua hiyo inafuatia hatua ya Askofu Mokiwa kumsimika Hotai juzi kuwa askofu wa Kanisa hilo Tanzania katika ibada maalum iliyofanyika katika Kanisa la Kristo jijini Arusha.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji aliyetoa katazo la kufanyika kwa sherehe za kumsimika Askofu Hotai, Kakusuro Sambo, alisema mahakama imethibitisha kuwa wadaiwa waliamua kwa makusudi kuidharau mahakama na kumsimika askofu kabla kutolewa kwa uamuzi juu ya zuio lililotolewa wiki iliyopita.
Jaji Sambo alisisistiza kuwa mahakama ilikubali kusikiliza maombi ya wadai ambao waliiomba kuzuia kufanyika kwa ibada hiyo kwa maelezo kuwa ingeathiri madai ya msingi ya walalalmikaji wanaotilia shaka umri wa askofu mteule wakidai kuwa alidanganya kuhusu umri wake.
Aidha, alisema mahakama ndio eneo ambalo linatoa haki na kwamba kitendo cha viongozi wa dini wa ngazi za juu kuidharau haivumiliki na kwamba hakuna aliye juu ya sheria, viongozi hao wawili wana kila sababau ya kuchukuliwa hatua kwa kuidharau mahakama.
Alieleza kuwa sheria za nchi zimeeleza wazi namna ya kushughulikia watu wanaoidharau mahakama bila kujali cheo wala nafasi waliyonayo katika jamii.
" Walichofanya viongozi hao yaani mdaiwa namba moja na mbili ni kinyume cha kifungu cha 114 sura ya 11 ya kanuni za adhabu katika vipengele C na K ambavyo vinaelekeza adhabu wanayostahili watu wanaoidharau mahakama," alisema.
Hoja ya kuchukuliwa kwa hatua viongozi hao wa dini ilitokana na Wakili wa wadai, De’suzer Junior, ambaye alidai mahakamani kuwa viongozi hao wamedharau mahakama kwa kumsimika Askofu Hotai, hatua ambayo imeharibu maslahi ya wateja wake katika kesi hiyo.
Wakili huyo alisema amri ya mahakama ya ngazi za juu inapaswa kuheshimiwa na kwamba viongozi hao wanastahili kuchukuliwa hatua.
Kabla ya kutolewa kwa amri hiyo, wakili wa utetezi, Joseph Tadayo, aliiomba mahakama kutupilia mbali hoja za upande wa wadai kwa kuwa zimewasilishwa mahakamani hapo bila kiapo, ambao ni utaratibu wa kuwasilisha hoja mahakamani. Tadayo pia, alidai kuwa wateja wake hawakumsimika askofu wa Dayosisi ya Mount Klimanjaro kama walivyokatazwa na mahakama bali Askofu Mokiwa alimwapisha Askofu Hotai kuwa askofu wa Anglikana nchini.
Alidai kuwa jambo hilo sio geni kwani hata makao makuu ya kanisa hilo Duniani nchini Uingereza hufanya hivyo.
Aliendelea kudai ibada iliyofanyika haikuwa ya kumsimika askofu wa dayosisi kwani ingelikuwa hivyo angeapishwa pamoja na wachungaji na walei wa kanisa hilo katika dayosisi.
Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na upande wa wadai, wakisema ibada hiyo ilifanyika katika eneo la makao makuu ya dayosisi hiyo na kadi za mialiko ya wageni waliohudhuria sherehe hiyo zilikuwa zinaonyesha wazi kuwa walikuwa wanafika hapo kushuhudia kusimikwa kwa Askofu Hotai.
Baada ya hoja za pande zote, Jaji Sambo alihitimisha hoja hizo kwa kusema kuwa mahakama imeridhika kuwa imedharauliwa na kwa kuwa nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria, ni lazima mahakama iheshimiwe na isidharauliwe.
" Kutokana na hatu hii naagiza mdaiwa namba moja na mbili wakamatwe na kufunguliwa mashtaka ya kuidharau mahakama," alihitimisha Jaji Sambo.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, baadhi ya waumini walionekana wakilia na simanzi kutawala eneo la mahakama.
MOKIWA: SINA TAARIFA ZA KUKAMATWA
Askofu Mokiwa alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana jioni, alisema hana taarifa zozote zinazohusu amri ya mahakama inayotaka akamatwe.
" Sina taarifa,” alijibu Askofu Mokiwa na kuongeza: “sijashtakiwa na sina kosa lolote." Hata hivyo, alimtaka mwandishi kuvuta subira ili afuatilie kwanza ukweli na undani kuhusu taarifa hizo.
No comments:
Post a Comment