May 21, 2011

MSAFARA WA MAALIM SEIF WAPATA AJALI



Na Mkwaya Remy

Gari iliyokuwa katika msafara wa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, imepata ajali.

Gari hilo lilipata ajali baada ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Noel Ernest, aliyekuwa akiendesha pikipiki kuingilia msafara wake.

Msafara huo wa Maalim Seif, ulikuwa ukitokea Wilaya ya Micheweni Kaskazini Pemba kwenda Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hassan Nassir, alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa askari huyo kuingia upande usio wake wakati gari ya msafara ikiwa katika mwendo wa kasi.

Alisema katika ajali hiyo, watu wanne walijeruhiwa akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Ali Mwinyikai.

Hata hivyo, anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu.

Aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali la Zanzibar Leo, Abdallah Mohammed, Mkurugenzi wa Utafiti wa Idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar, Mashaka Mwita na Mhasibu wa wizara hiyo, Iddi Mwita.

Kamanda Nassir alisema majeruhi hao walikuwa katika gari yenye usajili SLS 1143 aina ya Escudo ambayo iligonga mti wakati dereva akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki.

Hata hivyo, alisema majeruhi wawili, Ali Mwinyikai na Iddi, walisafirishwa kisiwani Unguja kwa matibabu zaidi.

Kamanda huyo alisema gari hiyo aina ya Escudo ni mali ya Shirika la Biashara Taifa (ZSTC) ilikuwa imewabeba viongozi hao waandamizi ambao wapo katika ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Alisema askari huyo wa JWTZ anafanyakazi katika kambi ya Ali Khamis na alikuwa akitokea mjini kwenda Vitongoji.

Alisema askari huyo pia alijeruhiwa na anaendelea kupatiwa matibabu akisubiri kuhojiwa na polisi.

Mwl Mkwaya
0777 052505

No comments:

Post a Comment