Mwl Remy Mkwaya via
Imechapwa 04 May 2011
NADHANI alikuwa Edda Sanga, mtangazaji wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD sasa TBC Taifa) ambaye aliendesha kipindi cha maswali na majibu mwaka 1981 kati ya Tabora Boys na Milambo sekondari.
Lengo la shindano lile la chemshabongo lililoandaliwa na RTD lilikuwa kupambanisha wanafunzi wa shule hizo mbili ambazo Mwalimu Julius Nyerere alisoma na kufundisha.
Nyerere alisoma Shule ya Sekondari Tabora Boys na alifundisha Milambo sekondari zote za mjini Tabora.
Katika shindano lililofanyika Tabora Boys, kila shule iliandaa vijana watano mabingwa wa kufikiri haraka na kujibu au waliosoma na kuhifadhi kichwani mafundisho.
Swali likatupwa kwa Milambo, “Uamuzi bora ni nini?” Swali jepesi sana, lakini liliwagalagaza mabingwa wote 10 wa kidato cha V na VI yaani watano wa Milambo na watano wa Tabora Boys. Edda akalitupa swali hilo kwa wasikilizaji.
Kijana wa kidato cha III kutoka Milambo sekondari alisimama na kujibu kuwa uamuzi wa busara ni hatua ya Mwalimu Nyerere kuacha kazi ya kuajiriwa (ualimu) na kufanya kazi ya siasa.
Mwanafunzi yule (nimesahau jina lake) alichagua kibao “Ndoa ya mateso” cha Marijan Rajabu kwa ajili ya burudani.
Ndiyo maana mpaka leo, walimu wanaojiamini hufanya ‘uamuzi wa busara’ kuacha kazi hiyo na kutafuta kazi nyingine, ikiwezekana hujiingiza katika masuala ya siasa - “kazi” yenye malipo ya ajabu.
Wengi wamefikishwa hapo kutokana na kupuuzwa na serikali, kukatishwa tamaa na mazingira ya kazi na tamaa ya maisha bora.
Walimu wengi ambao wangekuwa wanafundisha vijana leo wamechukua ‘uamuzi wa busara’ wakagombea na kuchaguliwa kuwa madiwani na wabunge.
Walimu wengi wametupa chaki wakachukua mafunzo mengine sasa ni wahariri wakuu wa vyombo vya habari au wafanyakazi katika mashirika na makampuni.
Ndiyo maana walimu kadhaa waliopangiwa vituo vya kazi Februari mwaka huu baada ya kukumbana na mazingira yasiyo rafiki kwao wakachukua posho za kujikimu na kuondoka.
Kulikoni? Katika siku chache walizokaa vituoni wakisubiri kulipwa fedha za kujikimu, walimu wapya wamekuwa wakisikia malalamiko yasiyoisha ya wenzao kutopandishwa madaraja kwa muda mrefu, wengine tangu 2004 hivyo wanaendelea kulipwa mishahara ileile ya wakati walipoanza kazi.
Aidha, wamesikia malalamiko ya waliopandishwa vyeo au madaraja lakini wakiendelea kulipwa mishahara ya zamani.
Mbali ya kusikia malalamiko ya walimu wenzao wanaodai malimbikizo ya mishahara, posho mbalimbali; wengine hawajalipwa fedha za uhamisho. Hizi ni kero sugu kwa walimu.
Katika hotuba yake ya kwanza alipoteuliwa kuchukua mikoba ya Edward Lowassa mwaka 2008, waziri mkuu, Mizengo Pinda aliangiza mwalimu asihamishwe kama hakuna fedha za uhamisho. Agizo hilo halifanyiwi kazi.
Kwa hiyo, japokuwa walimu waliochukua posho na kuacha kazi wamefanya kosa kisheria, lakini kuna mchango mkubwa wa serikali katika kosa hilo.
Tazama, waliporipoti hawakulipwa fedha za kujikimu, wengine walilipwa baada ya mwezi na zaidi. Serikali inadhani walimu walikuwa wanakula nini, mchwa au hewa?
Baadhi walikopa wakitarajia wakilipwa posho pamoja na mshahara wataweza kurudisha mikopo. Lakini baadhi waliambulia mshahara wa msaada wa Sh. 100,000 tu wakiambiwa wasubiri kuingizwa kwenye pay-roll.
Hata mwezi uliofuata majina ya walimu hayakuingizwa. Kwanini ualimu unafanywa ndoa ya mateso? Kwanini malalamiko ya mishahara ni kwa walimu tu na si idara nyingine?
Katika kipindi ambacho serikali imetoa vitisho kwa walimu ikitaka ama warejee kazini au warejeshe posho katika mwezi mmoja ujao, itakuwa busara ikatathmini upya wajibu wake kwa walimu. Kuufanya ualimu ndoa ya mateso, uamuzi wa busara ni kuacha kazi.
0777 05 25 05
ualimu ni ndoa ya mateso kati ya MWALIMU na mwajiri wake ambae kwa walimu wengi ni serikali.
ReplyDelete