May 19, 2011
NYAMBARI NYANGWINE ANYUKWA MAWE NA WANANCHI WAKE
Mbunge apigwa mawe
Na George Marato
Sare za CCM zachanwa
Magari nayo yapopolewa
Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwene (CCM)Hali katika kitongoji cha Nyamongo ni tete ikichangiwa na hisia kali za vifo vya watu watano waliouawa na Polisi kwa madai ya kutaka kuvamia mgodi wa North Mara, na sasa Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwene (CCM) na viongozi wengine wa halmashauri ya wilaya ya Tarime wameshambuliwa kwa mawe na magari yao kuharibiwa vibaya.
Tukio hilo lilitokea jana wakati Nyangwene akiwa na msafarawake wakiwasili Nyamongo katika mkutano uliokuwa umeitishwa kuzungumzia tukio la mauaji hayo, lakini miongoni mwa waliokuwamo kwenye msafara huo ni makada wa CCM waliokuwa wamevaa sare za chama hicho, hali iliyoamsha taharuki kubwa.
Wananchi hao kwa mamia walianza kupiga kelele kama vile kuomba msaada kutokana na kuvamiwa na wezi, huku wakilalamika kuwa waliokuwa wamevaa sare hizo walikuwa wanawakasirisha kwa kuwa serikali ya CCM imeshindwa kutatua kero zao.
Katika kadhia hiyo, kada mmoja wa CCM ambaye jina lake halikupatika mara moja, shati lake la chama lilichanwa chanwa, huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime, Amos Sagana, akivua sare ya shati na kofia za CCM na kubaki na fulana tu.
Makada wengine wa CCM aliokuwa wamevaa sare hizo, walilazimika kuzivua na kujisalimisha kwenye ofisi ya serikali ya mtaa katika eneo hilo.
Magari yaliyoharibiwa kwa kuvunjwa vioo ni la mwenyekiti wa halmashauri ya Tarime, Toyota Land Cruiser namba STK 8411 na la waandishi wa habari T299 ASW aina ya Toyota Land Cruser Prado mali ya mbunge huyo.
Yote yalipigwa kwa mawe yaliyokuwa yakirushwa mfululizo na wananchi jambo lilisababisha mbunge huyo na msafara wake kukimbia huku wakiendelea kushambuliwa.
Wananchi hao walieleza pia kwamba kitendo cha serikali kushindwa kuwapatia maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo pamoja na kushindwa kuchukua hatua za haraka katika kudhibiti mauaji ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakifanywa na polisi katika mgodi wa dhahabu wa North Mara ni moja ya sababu za kufanya hivyo.
“Sisi hatuna kosa na mbunge wetu kwanza yeye hakuua, lakini hatuwezi kumsikiliza kwa vile serikali yake ndio inayotumia polisi kulinda Wazungu na kutuua sisi kinyama kila kukicha,” alisema mwananchi mmoja.
Mwananchi mwingine alijitambilisha kwa jina la Chacha Keresa, alisema viongozi wa serikali katika ngazi ya wilaya wamekuwa wakishindwa kutatua matatizo yao, lakini wamekuwa wakijitokeza hadharani pindi tu wanaposikia wananchi wanakusudia kuwafanyia fujo wawekezaji.
“Siku zote sisi tunasema hatuna eneo la kulima tunataka tupewe sehemu ya kufanya uchimbaji mdogo, lakini umekuwa wimbo sasa leo wameuawa vijana wetu tena hata maiti zikiwa bado hazijazikwa wanakuja na nguo za CCM kufanya nini,” alisema.
Naye Yahana Chacha, alisema endapo serikali haitachukua hatua za haraka za kutatua tatizo la umaskini linalowakabili wananchi wa maeneo hayo hakuna amani itakayopatikana daima.
“Tunachosema hakuna jambazi anayekwenda kuiba mawe haya yote tunayafanya kwa umaskini sasa hapa si kutumia polisi bali serikali itafute njia ya kumaliza umaskini kwa wananchi bila hivyo wataleta hata JWTZ lakini hakuna watakachosaidia,” alisema.
Remy Mkwaya
0777 052505
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
kiongozi imara ni yule anayefhamu kwa dhati matatizo ya wananchi wake na kuyatafutia ufumbuzi wa dhati kuyatatua. Inasemekana Mwl. wa TZ alikuwa AMECHELEWA huko.
ReplyDelete